Mwili wa mwigizaji nguli wa humu nchini Winnie Bwire Ndubi uliwasilishwa nchini Jumapili Septemba 8, 2024 kutoka Istanbul Uturuki alikokwenda kutibiwa.
Babake mzazi kwa jina Edmond Kwena Ndubi aliyefika kwenye uwanja wa ndege wa Moi kisiwani Mombasa mapema kuupokea alisema ulikuwa umebebwa na ndege ya shirika la Ethiopian Airlines.
Kulingana naye, binti yake alipumzika baada ya kupambana na saratani ya matiti kwa muda mrefu ingawa alisalia mwenye ujasiri kwani hakuwahi kuwaonyesha machozi hata mara moja.
Mzee Ndubi alisema Winne ameacha pengo kubwa kutokana na talanta zake nyingi kama uigizaji, ufunsi wa samani, uokaji na uimbaji.
“Sisi kama familia tunaweza tu kusema kwamba ni vizuri Winnie amepumzika, kwa sababu kwa wale huenda hamjui aliteseka sana.” Alisema Mzee huyo huku akishukuru kila mmoja aliyetoa mchango wake ili kufanikisha matibabu yake.
Winnie Ndubi alikuwa akiugua saratani ya matiti na aliwahi kuenda Uturuki mara ya kwanza kwa matibabu na alistahili kurejea kuona daktari wake lakini akagonjeka ndiposa akapelekwa.
Wasanii waliofika kwenye uwanja wa ndege kupokea mwili wake waliitaka serikali kuhakikisha kwamba gharama ya matibabu ya saratani inapunguzwa na yawe yanapatikana nchini.
Mwili huo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya Pandya huko Mombasa na kulingana na babake mazishi huenda yakaandaliwa tarehe 21 mwezi huu nyumbani kwao magharibi mwa Kenya.