Home Burudani Mwigizaji wa Nollywood Cynthia Okereke ameaga dunia

Mwigizaji wa Nollywood Cynthia Okereke ameaga dunia

0

Mwigizaji wa muda mrefu kwenye filamu za Nigeria almaarufu Nollywood Cynthia Okereke ameaga dunia.

Taarifa kuhusu kifo chake zilitolewa kwenye mitandao ya kijamii na J.C. Okechukwu ambaye ni mwandalizi wa filamu nchini Nigeria. Okechukwu alichapisha picha ya Cynhtia ambaye alikuwa na umri wa miaka 63 na kuandika ujumbe wa “Lala salama” huku akisema kifo hicho kimemvunja moyo.

Kulingana na Okechukwu, Cynthia alikata roho usiku wa kuamkia Jumatano 12, Julai, 2023 akiwa usingizini.

Mwandalizi huyo wa filamu anaelezea kwamba alikuwa anajiandaa kumsafirisha mwigizaji huyo ili wamalizie kazi ambayo walikuwa wameanzisha wakati alipata habari za kifo chake.

“Naomba niweze kupona kutokana na mshtuko huu. Maisha kweli ni ukungu. Dakika moja unayo, dakika nyingine hauna,” aliandika mwandalizi huyo wa filamu.

Mwisho wa mwezi Julai mwaka 2022, Cynthia Okereke na mwigizaji mwenza Clemson Cornel Agbogidi walitekwa nyara walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka eneo la kuandaa filamu, mjini Ozala, jimboni Enugu. Baadaye wawili hao walipatikana wakiwa hafifu.

Inaaminika kwamba mama huyu hakuwahi kupona kutokana na aliyoyapitia wakati alikuwa ametekwa nyara.

Cynthia Nkiru Okereke alizaliwa mwaka 1960, na alianza kuigiza mwaka 1998, kwenye filamu iitwayo “King Jaja of Opobo”.

Alijipatia umaarufu kwenye tasnia ya uigizaji ndani na nje ya Nigeria baada ya kuigiza kama “Sofia” kwenye filamu “Usofia in London” pamoja na Nkem Owoh. Ameigiza kwenye filamu nyingine nyingi zikiwemo “Hidden Tears”, “Sound of Love”, “Coronation”, “Second Burial”, “Lion Finger” na “Second Chance”

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here