Mwigizaji wa Marekani James Earl Jones amefariki akiwa na umri wa miaka 93. Kulingana na familia yake alikata roho asubuhi ya Jumatatu Septemba 9, 2024 kulingana na saa za Marekani.
Jones aliyehusika kwenye filamu nyingi kama vile “Field of Dreams”, “Coming To America”,” Conan the Barbarian” na “The Lion King” alifariki akiwa amezingirwa na wapendwa wake.
Aliwahi kujishindia tuzo kadhaa kama mwigizaji zikiwemo tatu za Tony, mbili za Emmy na moja ya Grammy. Waandalizi wa tuzo za Oscar mwaka 2011 nao walimtunuku tuzo ya heshima ya mafanikio maishani.
Aliweka historia ya kuwa mwigizaji wa pili wa kiume wa asili ya Afrika au ukipenda mmarekani mweusi kuwahi kuteuliwa kuwania tuzo ya mwigizaji bora kwenye tuzo za Oscar mwaka 1971. Wa kwanza alikuwa Sidney Poitier.
Waigizaji wenzake wamekuwa wakitoa pole zao kupitia mitandao ya kijamii huku wengine wakisimulia waliyotangamana naye kikazi na watakavyomkosa.
LeVar Burton alikuwa mmoja wa waigizaji wa kwanza kutoa ujumbe kama huo akisema kamwe hakutawahi kuwa na mwigizaji mwingine ambaye atakuwa na talanta na neema kama yake.
Colman Domingo aliandika, “Asante sana James Earl Jones kwa kila kitu. Mtaalamu wa uigizaji. Tunasimama kwenye mabega yako. Pumzika sasa. Ulitupa mazuri yako.”.
Kevin Costner ambaye aliigiza na Jones kwenye kazi “Field of Dreams” alimsifia mwendazake akisema alikuwa na sauti ya kipekee, uwezo, ukarimu na kwamba ni mengi yanaweza kusemwa kuhusu urithi wake.
“Kwa hivyo nitasema tu kuhusu jinsi ninashukuru kwa kuwa sehemu ya urithi huo unaojumuisha ‘Field of Dreams’.” alimalizia Costner.
Marehemu Jones ameacha mwanawe mmoja kwa jina Flynn Earl Jones wa umri wa miaka 42.
Aliwahi kuwa kwenye ndoa na Julienne Marie kati ya mwaka 1968 na 1972 wakajaliwa mtoto Flynn kisha akamwoa Cecilia Hart mwaka 1982 wakatengana mwaka 2016.