Home Habari Kuu Mwenyekiti mpya wa AUC kutoka Afrika Mashariki

Mwenyekiti mpya wa AUC kutoka Afrika Mashariki

Kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga, tayari ameelezea nia ya kuwania wadhifa huo na ameungwa mkono na Rais William Ruto katika azima yake hiyo.

0

Baraza Kuu la Umoja wa Afrika, AU leo Ijumaa limeidhinishaa kwa kauli moja kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC atachaguliwa kutoka Afrika Mashriki. 

Kufuatia uamuzi huo, Afrika Mashariki imetakiwa kuwasilisha wagombea watakaowania wadhifa huo wakati wa uchaguzi utakaondaliwa mwezi Februari mwaka 2025.

“Huu ni ushindi mkubwa kwa eneo la Afrika Mashriki kuwasilisha wagombea wa wadhifa wa mwenyekiti wa AUC,” alisema Musalia Mudavadi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya punde baada ya kufikiwa kwa uamuzi huo.

Kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga, tayari ameelezea nia ya kuwania wadhifa huo na ameungwa mkono na Rais William Ruto katika azima yake hiyo.

Marais Yoweri Museveni wa Uganda, Samia Suluhu wa Tanzania na Paul Kagame nao pia wameripotiwa kumuunga mkono Raila kugombea wadhifa huo.

“Ni wazi kuwa Mheshimiwa Raila Odinga atakuwa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika,” aliongeza Mudavadi aliyeshawishi mno Baraza Kuu la AU kuidhinisha uamuzi kwamba mgombea wa AUC anapaswa kutoka Afrika Mashariki.

Uamuzi huo ni kwa mujibu wa sheria ya AUC, sheria za utaratibu wa taasisi za sera za AU na uamuzi wa Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali.

Kadhalika, ilikubaliwa kwamba eneo la Kaskazini mwa Afrika litoe wagombea wa wadhifa wa Naibu Mwenyekiti wa AUC huku maeneo mengine matatu ya Kati, Kusini na Magharibi mwa Afrika yakipewa fursa ya kujaza nyadhifa sita za makamishna wa tume hiyo.

Hadi kufikia sasa, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Somalia Fawzia Yusuf Adam ametangaza nia ya kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa AUC.

Mwenyekiti wa sasa wa AUC ni Moussa Faki Mahamat kutoka Chad ambaye muda wake wa kuhudumu utamalizika mapema mwaka 2025.

Website | + posts