Mwanzilishi wa bendi ya maarufu hapa nchini ya Them Mushrooms Teddy Kalanda, ameaga dunia.
Kalanda pamoja na ndugu zake wawili Billya Sarro na George Zirro, walianzisha bendi hiyo mwaka 1972.
Kalanda alifariki kutokana na saratani, ugonjwa ambao amekabiliana nao kwa muda wa miaka sita iliyopita.
Kaka yake John Katana, alithibitisha kifo hicho, akisema kuwa imekuwa safari yenye uchungu mwingi kwa ndugu yake ambaye amekuwa kielelezo kwao.
Awali bendi hiyo ilijulikana Avenida Success, iliimarisha umaarufu wake baada ya kubadilisha jina na kuwa Them Mushrooms.
Bendi hiyo ilizidi kuwa chaguo bora kwa wengi husasn baada ya kutoa wimbo ‘Jambo Bwana’ mwaka 1982, uliopendwa sana kutokana na kauli mbiu yake “Hakuna Matata”.
Kalanda alifariki akiwa nyumbani kwake katika kaunti ya Kilifi, akiwa na umri wa miaka 72.