Mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegie, aliyekuwa akipokea matibabu nchini Kenya baada ya kuchomwa moto na mpenzi wake, ameaga dunia.
Kupitia mtandao wa X Alhamisi alfajiri, shirikisho la riadha nchini Uganda (UAF) lilithibitisha kifo cha Cheptegie, huku likishutumu kisa hicho na kutoa wito wa haki kupatikana.
“Tuna huzuni kutangaza kifo cha mwanariadha wetu Rebecca Cheptegei kilichotokea leo asubuhi kutokana na mzozo wa kinyumbani. Kama shirikisho tunalaani kisa hicho na tunatoa wito wa haki kupatikana,” ilisema UAF.
Cheptegie, alikuwa akipokea matibabu katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi mjini Eldoret, baada ya mwili wake kuchomeka asilimia 80.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33, alishambuliwa Jumapili na mpenzi wake Dickson Ndiema Marangach, aliyemvizia nyumbani kwake katika kaunti ya Trans Nzoia, kabla ya kumwagia mafuta ya petroli na kumteketeza.
Kulingana na maafisa wa polisi Marangach, pia alipata majeraha mabaya ya moto katika kisa hicho.
Wazazi wa mwanariadha huyo waliotoka nchini Uganda kumtembelea mwanao, walisema Cheptegie alinunua nyumba na shamba nchini Kenya, ili iwe rahisi kwake kufanya mazoezi.