Home Burudani Mwanamuziki wa Uganda Adam Mulwana afariki

Mwanamuziki wa Uganda Adam Mulwana afariki

0

Mwanamuziki wa taifa jirani la Uganda Adam Mulwana ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 36, baada ya kuugua kwa muda mfupi kulingana na familia yake.

Mulwana anafahamika sana nchini Uganda kwa wimbo wake uitwao “Toka Kwa Barabara” alioimbwa kwa ajili ya kampeni ya mwaniaji urais Daktari Kizza Besigye miaka ya 2010 na 2011.

Msajiliwa huyo wa kampuni ya muziki ya “Cream production” ana nyimbo nyingine kama ‘Kampala Ayola’ na ‘Esala ya Kabaka’ pamoja na nyingine nyingi ambazo hazikuchezwa kwenye vyombo vya habari nchini Uganda.

Mzaliwa huyo wa eneo la Buziranduulu, wilaya ya Luweero alishangaza wengi miezi kadhaa kabla ya kifo chake aliposimulia jinsi alitiliwa sumu na mwanamke fulani.

Kulingana naye, alikutana na mama huyo aliyejisingizia kuwa shabiki wake kutoka Marekani akiwa na watoto wawili katika mkahawa mmoja eneo la Makindye, jijini Kampala.

Alipofika eneo la mkutano aliwapata watatu hao wakiwa tayari wameagiza Pizza wakala na wakabakisha vipande vitatu.

Mwanamke huyo anasemekana kulazimisha Adam kula vipande hivyo akakataa lakini akamlazimisha na mtoto mmoja alipojaribu kuchukua kipande kimoja mama huyo akapiga mkono wake na kuchukua vipande hivyo na kuviweka kwenye mkoba wake.

Baada ya mkutano, Adam alikabidhiwa dola 300 na mwanamke huyo.

Alidai kukumbuka matukio hayo baadaye na kuelezea kwamba mama huyo alikuwa wa asili ya Rwanda na watoto aliokuwa nao hawakuwa wake na kwamba huenda alitumwa na mtu kumtilia sumu.

Website | + posts