Mwanamuziki maarufu wa Afrika Kusini Zahara ambaye jina lake halisi ni Bulelwa Mkutukana ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 35.
Zahara alifariki wakati akipokea matibabu katika hospitali moja ya kibinafsi jijini Johannesburg.
Taarifa za kifo cha mwanamuziki huyo aliyefahamika sana kutokana na albamu yake iliyofahamika kama “Loliwe,” zilitangazwa na Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni wa nchi hiyo Zizi Kodwa.
“Nahuzunishwa mno kutokana na kifo cha @ZaharaSA. Salamu zangu za rambirambi kwa familia ya Mkutukana na tasnia ya muziki nchini Afrika Kusini. Serikali imekuwa na familia kwa muda hadi kufikia sasa. Zahara na gita yake aliacha kumbukizi isiyofutika katika muziki wa Afrika Kusini,” alisema Waziri Kodwa kupitia mtandao wa X.
Familia yake bado haijatoa taarifa rasmi kuhusu chanzo cha kifo chake ingawa taarifa zinasema alifikishwa hospitali hapo akilalamikia kuumwa na mwili.
Taarifa zingine ambazo hazijathibitishwa zinaashiria Zahara alikuwa na matatizo ya ini.
Katika mitandao ya kijamii, Zahara ameombolezwa duniani kote huku wengi wakimtaja kama mwanamuziki aliyegusa nyoyo za wengi kutokana na ubabe wake wa kucheza gita wakati sauti yake ya inga ikitikisa kila pembe ya anga.