Home Habari Kuu Mwanaharakati Bonface Mwangi ahukumiwa kwa kudharau mahakama

Mwanaharakati Bonface Mwangi ahukumiwa kwa kudharau mahakama

0

Mwanaharakati wa humu nchini Boniface Mwangi amehukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani au faini ya shilingi laki 3 baada ya kupatikana na kosa la kudharau mahakama.

Makosa hayo yanatokana na kesi iliyowekwa dhidi yake na waziri wa utalii na wanyamapori Daktari Alfred Mutua.

Mwangi ambaye alikwenda mahakamani leo akiwa ameandamana na wakili Martha Karua alisema kwamba agizo la mahakama linalomzuia kuzungumza juu ya kuharibiwa kwa nyumba yake limeongezwa muda hadi Januari 2024.

Mwanaharakati huyo alitumia mtandao wa X ambao wakati huo ulifahamika kama Twitter kuelezea kuhusu kushambuliwa kwa nyumba aliyokuwa akijenga huko Machakos kwa bomu.

Ujumbe huo wa Oktoba 21, 2021 ulielezea kwamba mjengo huo ulizama kufuatia uvamizi huo na wafanyakazi waliokuwepo waliibiwa.

Aliendelea na maelezo yake ambapo alimtaja Mutua ambaye wakati huo alikuwa akihudumu kama gavana wa gatuzi la Machakos, kama mshukiwa mkuu.

Mutua alimshtaki Mwangi kupitia kwa wakili wake kutokana na madai hayo akisema alimharibia jina.

Amesema kwamba atalipa faini huku akishikilia wazo kwamba mbaya wake ni Alfred Mutua.

Kupitia mtandao huo huo wa X, Mwangi amelalamika kuhusu idara husika kukosa kuchukua hatua ilhali ametoa ushahidi wote unaohitajika.

Alichapisha ujumbe huo leo hata baada ya agizo la kumzuia kuzungumzia suala hilo kuongezwa muda.

Website | + posts