Home Kaunti Mwakilishi Wadi ya Lakezone, kaunti ya Turkana afariki

Mwakilishi Wadi ya Lakezone, kaunti ya Turkana afariki

0

Michael Egialan Ekwar ambaye ni Mwakilishi Wadi ya Lakezone katika kaunti ya Turkana amefariki.

Spika wa bunge la kaunti ya Turkana Christopher Nakuleu alithibitisha hayo akielezea kwamba Egialan ambaye alikuwa akipambana na saratani ya umio kwa zaidi ya mwaka mmoja, alikata roho akipokea matibabu katika hospitali ya St. Lukes mjini Eldoret.

Nakuleu alimwomboleza mwakilishi huyo akimtaja kuwa kiongozi aliyejitolea kutumikia wananchi na ambaye mchango wake ulihisiwa katika kaunti na katika taifa.

Spika huyo alitoa rambirambi zake na watendakazi wote wa bunge la kaunti ya Turkana kwa ndugu, jamaa na marafiki wa mwendazake pamoja na wakazi wote wa wadi hiyo ya Lakezone.

Aliahidi msaada wa bunge la kaunti ya Turkana kwa familia yake wakati huu wa majonzi.

Egialan alichaguliwa kama Mwakilishi Wadi ya Lakezone kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana na alihusika pakubwa katika kupitishwa kwa sheria kadhaa za manufaa kwa watu wa kaunti ya Turkana.

Alikuwa akihudumu kama naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge hilo kuhusu kilimo, mifugo na uchumi wa ufugaji.

Awali, alihudumu kama naibu chifu wa lokesheni ndogo ya Kokuro, chifu wa lokesheni ya Lowareng’ak na mwenyekiti wa kamati ya hazina ya maendeleo, CDF katika eneo bunge la Turkana Kaskazini.