Watu kadhaa walifariki kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika kaunti ya Nairobi jana Jumapili usiku.
Gavana Johnson Sakaja anasema miongoni mwa waliofariki ni polisi mmoja aliyekuwa akiwaokoa watu wasiopungua wanne katika eneo la Kamukunji.
Familia kadhaa katika maeneo ya Waruku, Kasarani na Dandora pia ziliwapoteza wapendwa wao kutokana na mvua hiyo.
“Kwa familia hizi ambazo zimewapoteza wapendwa wao nasema poleni sana. Nawaombea nguvu wakati huu mgumu,” alisema Sakaja katika taarifa.
Kufuatia mvua hiyo, serikali ya kaunti ya Nairobi imetaja maeneo kadhaa kuwa yaliyoathirika ikiwa ni pamoja na Kangemi, Mukuru kwa Reuben na Kwa Njenga, Kware, Kamukunji, Viwandani, Kayole na Njiru.
Gavana Sakaja akisema serikali yake itahakikisha wakazi wa maeneo hayo wanapata maji safi ya kunywa, mitaro inaondolewa taka na watu wasiojulikana waliko kutafutwa.
Barabara kadhaa pia ziliathiriwa na mvua hiyo iliyonyesha usiku kucha na kutatiza usafiri wa magari na watu.
Barabara hizo ni pamoja na Peponi, Ojijo, Bunyala, Bunyala, Baricho, Jogoo na barabara ya mwendokasi ya Nairobi Express way.