Home Habari Kuu Muungano wa Azimio waipa serikali saa 48 kumaliza mgomo wa madaktari

Muungano wa Azimio waipa serikali saa 48 kumaliza mgomo wa madaktari

0

Muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya umeipa serikali makataa ya saa 48 imalize mgomo unaoendelea wa madaktari la sivyo ikabiliwe na mgomo wa kitaifa.

Kalonzo Musyoka ambaye ni mmoja wa vigogo wa muungano huo alihutubia wanahabari jijini Nairobi ambapo alishauri serikali kutumia muda wa siku mbili ambao ilipatiwa na mahakama kuafikia makubaliano na madaktari.

Alitishia kwamba iwapo serikali itakosa kutatua mgomo huo kwa muda wa siku mbili, upinzani utahamasisha miungano ya wafanyakazi na wananchi kwa jumla kutekeleza mgomo wa kitaifa.

Taarifa ya pamoja ya muungano huo inasema kwamba kufikia sasa, serikali haijadhihirisha kujitolea kutatua mgomo wa madaktari.

Wakati huo huo Upinzani unataka serikali itangaze mafuriko kuwa janga la kitaifa na kuongeza mgao wa fedha kwa waathiriwa kutoka shilingi bilioni 1 hadi bilioni 7.

Wanasiasa hao wa upinzani wamemlaumu Rais Ruto kwa kile walichokitaja kuwa kuamuru ubomozi wa makazi ya waathiriwa na kuondolewa kwa lazima katika maeneo yao bila kuwapa makazi mbadala.

Kuhusu waziri wa kilimo Mithika Linturi ambaye kesi ya kutaka kumwondoa afisini inasikilizwa katika bunge la taifa, upinzani unataka mchakato wa kumwondoa afisini uharakishwe na kamati husika itekeleze matakwa ya hoja ya kumwondoa afisini.

suala lingine aliloligusia Kalonzo ni kifo cha Jenerali Francis Ogolla kwenye ajali ya ndege ambapo alitaka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu ajali hiyo.

Website | + posts