Viongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wametangaza kwamba maandamano yataendelea kama ilivyopangwa kesho Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki hii.
Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga jijini Nairobi, viongozi hao waliwataka maafisa wa polisi kutoa ulinzi kwa waandamanaji.
Mabalozi wa nchi za kigeni nchini awali walitoa taarifa ya kuomba upinzani kusitisha maandamano na kushiriki mazungumzo.
Jana Jumatatu, wabunge wa mrengo wa upinzani walitoa taarifa ya pamoja kusema kwamba maandamano yataendelea jinsi ilivyopangwa hadi pale ambapo serikali itaridhia matakwa yao.
Wabunge hao walitaja maandamano hayo kuwa halali kwa mujibu wa kifungu nambari 37 cha katiba.
Aidha walisema mchakato wa kukusanya sahihi za Wakenya unaendelea na pia unalindwa na kifungu cha kwanza cha katiba kinachosema mamlaka yote ni ya wananchi.
Viongozi wa upinzani bungeni wamekosoa mtazamo wa serikali kuhusu maandamano ya awali kwamba waandamanaji waliojitokeza katika sehemu mbalimbali za nchi walilipwa. Walisema kwa kudhania hivyo, serikali haitaki kukubali hali halisi na ni dhana hatari kwa nchi.
Walisema serikali haifahamu jinsi Wakenya wamekasirika na walivyo na njaa wakati inadai kwamba maandamano hayakuchochewa na gharama ya juu ya maisha. Kulingana nao, serikali haioni kama gharama ya maisha iko juu kiasi cha kuwafanya Wakenya waandamane.
Waliilaumu serikali kwa kukwama kwenye maridhiano ya mwaka 2018 kati ya Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ikisema kwamba ana njama ya kuingia kwenye serikali kupitia maridhiano sawia.
Serikali imeonya dhidi ya maandamano ya upinzani kwani waandamanaji wanaharibu mali ya umma na ya Wakenya binafsi.