Home Kaunti Murkomen: Serikali itawahamisha wanabiashara walio kando ya barabara kuu

Murkomen: Serikali itawahamisha wanabiashara walio kando ya barabara kuu

0

Waziri wa uchukuzi Kipuchumba Murkomen, amesema serikali itawahamisha wachuuzi na masoko ya wazi kutoka barabara kuu.

Murkomen aliyasema hayo Jumamosi asubuhi katika eneo la Londiani kaunti ya kericho, ambapo watu 52 walifariki na wengine 35 kujeruhiwa baada ya trela kugonga magari kadhaa katika makutano ya Londiani katika barabara kuu ya Kericho-Nakuru Ijumaa jioni.

Kulingana na waziri Murkomen, Gavana wa kaunti ya Kericho Dkt. Eric Mutai amejitolea kutafuta ardhi ambapo soko hilo litahamishiwa.

“Serikali ya kitaifa ina mipango ya kupiga jeki ujenzi wa masoko ya kisasa kote nchini. Watu wengi watanufaika na masoko hayo yakijengwa karibu na barabara, lakini sio katika ardhi iliyotengewa upanuzi wa barabara,” alisema Murkomen.

Na katika juhudi za kuepusha ajali sawia na hiyo siku za usoni, waziri Murkomen alisema matuta ya barabarani yatawekwa, ili kupunguza mwendo wa magari katika eneo hilo.

Kamanda wa polisi wa Londiani Agnes Kunga aliyezungumza na shirika la utangazaji la KBC, alisema polisi wanamsaka dereva wa lori hilo lenye nambari za usajili za Rwanda, aliyetoweka baada ya ajali hiyo.

Wafanyabiashara wakiwemo wahudumu wa bodaboda ambao huendesha shughuli zao katika kituo hicho, ni miongoni mwa walioangamia kwenye ajali iliyotokea Ijumaa  saa kumi na mbili jioni.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here