Home Burudani Mulamwah aamua kutumia sheria kuona mwanawe

Mulamwah aamua kutumia sheria kuona mwanawe

0

Mchekeshaji Mulamwah ameamua kufuata mkondo wa sheria ili kuweza kuona mtoto wake na hata kuwa kwenye maisha yake na kutekeleza majukumu yake kama baba.

Mulamwah ambaye jina lake halisi ni David Oyando alichapisha nakala za barua za mawakili wake kwa mzazi mwenzake Carol Muthni kwenye Instagram.

“Mambo ni mahakamani sasa. Diplomasia ilikosa kufanya kazi sasa tujaribu sheria.” aliandika Mulamwah huku akihimiza wafuasi wake kutokuwa wepesi wa kumnyoshea kidole cha lawama.

Mulamwah na aliyekuwa mpenzi wake Carol “Sonnie” Muthoni walibarikiwa na mtoto wa kike kwa jina Keilah Oyando na kutengana muda mfupi baada ya kuzaliwa kwake.

Analalamika kwamba hajakuwa akipata fursa ya kuwa katika maisha ya mwanawe kwani hata akituma pesa za matumizi kwa mama mtoto zinarejeshwa.

Katika barua hiyo ya mawakili wa Mulamwah kwa Sonnie, Mulamwah anataka Sonnie akome kumtaja kwenye mahojiano na kwenye mitandao ya kijamii.

Anatakiwa pia kuhakikisha kwamba mazungumzo kati yake na baba mtoto yawe tu kuhusu mtoto wao na wala sio suala jingine.

Ili kusaidiana katika malezi ya Keilah, Sonnie anatakiwa kumpa Mulamwah mtoto huyo kwa siku mbili zinazofuatana yapata mara mbili kwa mwezi ambapo inapendekezwa iwe kati ya Ijumaa na Jumapili saa kumi na moja jioni.

Cheti cha kuzaliwa cha mtoto huyo kinafaa pia kutolewa kwa baba mtoto ili aweze kumtengenezea pasi ya usafiri na kumweka kwenye bima ya afya.

Hafai pia kumhusisha mtoto kwenye matangazo ya kibiashara bila idhini ya babake.

Mulamwah baada ya kuachana na Carol Sonnie ana mpenzi mwingine ambaye pia yuko karibu kujifungua.