Home Kaunti Mueke: Mswada wa Ufugaji 2024 utastawisha sekta ya mifugo nchini

Mueke: Mswada wa Ufugaji 2024 utastawisha sekta ya mifugo nchini

Wakulima wengi wamepinga mswada huo unaoharamisha uuzaji wa vyakula vya mifugo bila leseni miongoni mwa masuala mengine muhimu aliyoyazungumzia.

0
Katibu katika idara ya ustawi wa mifugo Jonathan Mueke azindua zoezi la chanjo ya mifugo, kaunti ya Embu.
kra

Katibu katika idara ya ustawi wa mifugo Jonathan Mueke, ametetea Mswada wa ufugaji wa mwaka 2024, akiwahakikishia wafugaji kuwa unanuiwa kuimarisha ubora wa aina ya mifugo nchini.

Akiongea katika eneo la  Mbeere Kusini, Kaunti ya Embu, wakati wa shughuli ya uzinduzi wa chanjo ya mifugo inayoendelea kote nchini, Mueke alitaja sekta mbalimbali zinazopewa kipaumbele na idara yake, kama vile ustawi wa ufugaji na usambazaji wa vifaa vya kuhifadhi na kuandaa maziwa vinavyohitajika mno na wakulima wa mifugo.

kra

Matamshi ya Mueke yanajiri baada ya bunge la taifa kukatalia mbali mswada huo ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza kwenye bunge hilo, juma lijalo.

Akikatalia mbali Mswada huo, kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa aliye pia mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa, alisema idara ya ustawi wa mifugo, haikuhusisha umma vilivyo katika utayarishaji wa Mswada huo.

Hata Hivyo Mueke amesema atahamasisha wakulima kufahamu kuwa mswada huo unalenga kuwalinda kwa kuhakikisha wanapata mbegu bora za mifugo, kulingana na mazingira yao.

“Tutaendelea kuwafahamisha wakulima kuwa mswada huu unawalinda, kwa kuwawezesha kupata mbegu bora za mifugo,” alisema katibu Mueke.

Wakulima wengi wamepinga mswada huo unaoharamisha uuzaji wa vyakula vya mifugo bila leseni miongoni mwa masuala mengine muhimu aliyoyazungumzia.

Aidha, Mueke alifichua kwamba kampeni ya chanjo ya kitaifa inanuia kuwachanja ng’ombe milioni 22 pamoja na mbuzi na kondoo milioni 50 kote nchini, akisema serikali imejitolea kuhakikisha afya na usalama wa mifugo inazingatiwa katika Kaunti hiyo ili kuboresha uchumi na biashara za wakazi wa eneo hilo.

Website | + posts