Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi, amewahakikishia wakenya kwamba mazungumzo baina ya serikali na upinzani yataangazia masuala yanayowaathiri wakenya na wala sio mkataba wa kugawana mamlaka.
Akiongea katika shule ya upili ya Muslim kaunti ya Kakamega, Mudavadi alisema mazungumzo hayo yataangazia masuala matano muhimu yaliyopendekezwa ili kuhakikisha amani inadumishwa hapa nchini.
Hayo yalijiri huku spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula, akisema anaunga mkono mazungumzo hayo yanayoendelea, akitambua wajibu muhimu wa mazungumzo hayo katika kudumisha amani kote nchini.
Wetangula alisema anaridhia uamuzi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wa kusitisha maandamano, akisema mazungumzo na wala sio fujo, ndiyo yatakayosaidia kutatua changamoto zinazoshuhudiwa hapa nchini.
Spika huyo alitoa wito kwa wakenya wawe na subira na kumpa rais muda wa kutekeleza mipango yake kwa taifa hili.