Kenya itaendelea kuimarisha uhusiano mwema na Somalia katika maeneo yote yenye maslahi ya pamoja, ili kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi hizo mbili, amesema waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi.
Mudavadi, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje na maswala ya ughaibuni, alidokeza kuwa ushirikiano kati ya Nairobi na Mogadishu, utazingatiwa katika misingi dhabiti na kwa nia njema.
“Tutaendelea kufurahia uhusiasno mwema ulio na mizizi katika historia sawa, turathi na mipaka ya pamoja na ushirikiano wa uchumi,” alisema Mudavadi.
Mudavadi aliyasema hayo Jumatatu, wakati wa kikao cha tatu cha tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Kenya na Somalia, Jijini Nairobi.
“Sio kwa sababu tuna mpaka wa pamoja, lakini ni kwa sababu tuna ushirikiano thabiti tangu nchi hizi mbili zilipobuni uhusiano wa kidiplomasia katika miaka ya 60,” alidokeza Mudavadi.
Mudavadi alisema serikali zinazoshirikiana, huwapa changamoto raia wake kuiga mfano huo, kwa lengo la kupanua uhusiano wao.
Aidha waziri huyo alisema kuwa tume hiyo ya pamoja, ni mojawapo wa ushirikiano bora zaidi wa pande mbili katika siku za usoni.