Home Habari Kuu Mudavadi: China imekuwa mshirika wa kutegemewa

Mudavadi: China imekuwa mshirika wa kutegemewa

0

Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amepongeza ushirikiano mzuri uliopo kati ya Kenya na China anaosema umesaidia kuhuisha ustawi wa nchi zote mbili. 

Ametoa wito wa ushirikiano huo kuboreshwa zaidi ili kuafikia upeo wa maendeleo kwa manufaa ya watu wa mataifa hayo.

“Uhusiano kati ya Kenya na China una historia nzuri ya miaka 60, ambayo inalingana na uhuru wa nchi yetu. China imekuwa moja ya washirika wetu wa zamani zaidi na wakubwa tangu Kenya ijinyakulie uhuru. Kenya inathamani mno uhusiano mzuri na wa kihistoria ilio nao na China uliojengwa kwa misingi ya uaminifu, manufaa ya pande mbili na kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine,” aliongeza Mudavadi wakati wa sherehe za kuamdhimisha miaka 74 tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China.

Sherehe hizo zilifanyika katika ubalozi wa China nchini Kenya leo Alhamisi asubuhi.

Mudavadi aliiwakilisha serikali ya Kenya na raia wake wakati wa hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge la Taifa Gladys Shollei na Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati.

Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman pia alihudhuria sherehe hizo.

Uhusiano mzuri kati ya Kenya na China umechangia maendeleo mbalimbali nchini, hususan ujenzi wa barabara ya mwendokasi ya Nairobi Expressway na reli ya kisasa ya SGR.

Kadhalika nchi hizo mbili zinashirikiana katika nyanja mbalimbali kama vile elimu, na tayari Kichina kinafunzwa katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Kenya mathalan Chuo Kikuu cha Nairobi wakati wanafunzi Wakenya wakisomea nchini China katika mpango wa mabadilishano unaolenga kuboresha uhusiano kati ya Kenya na China..

“Tunapongeza uwekezaji mkubwa wa moja kwa moja wa kigeni unaofanywa na China hasa katika miradi ya miundombinu. Hebu tuendelee kuboresha uhusiano wetu, kuimarisha ushirikiano, na kutafuta fursa za pamoja kwa ajili ya ukuaji wa pande mbili,” alisema Mudavadi wakati wa hafla iiliyoandaliwa na kuhudhuriwa na maafisa mbalimbali wa ngazi ya juu wa China wakiongozwa na Balozi wao nchini Kenya Zhou Pingjian.
Pingjian aliahidi kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na China na kutetea maslahi ya nchi zote mbili.
Website | + posts