Home Habari Kuu Mudavadi awaonya wafisadi, asema watachukuliwa hatua kali

Mudavadi awaonya wafisadi, asema watachukuliwa hatua kali

0

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amesema kuwa ufisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma havitakubaliwa katika serikali ya Kenya Kwanza. 

Amewataka Wakenya kutupilia mbali uovu huo na kuwa raia wanaotii sheria.

“Nchi nzuri ni ile inayoheshimu utawala wa sheria na isiyokuwa na ufisadi. Unapopewa fursa ya kutumikia nchi, kuwa mtumishi wa watu na siyo mtu anayetaka kutimiza maslahi ya kibinafsi badala ya kuwatumikia Wakenya,” alisema Mudavadi wakati akiongoza tamasha ya utamaduni mjini Vihiga.

Na huku Wakenya wakihangaika kutokana na gharama ya juu ya maisha, Mudavadi alisema serikali inafanya jitihada za kimakusudi kuwaondolea Wakenya mzigo huo.

Amewataka kuwa na subira akielezea matumaini kuwa hatimaye itavuta heri.

“Wito wangu kwa Wakenya ni kwamba hata tunapouaga mwaka wa 2023, waendelea kuwa na matumaini na kuunga mkono sera za serikali. Serikali ina kusudi bora kwa Wakenya,” aliongeza Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.