Home Habari Kuu Mudavadi atua Uswizi kwa ziara ya siku tatu

Mudavadi atua Uswizi kwa ziara ya siku tatu

0

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi amewasili mjini Geneva nchini Uswizi wakati akiimarisha juhudi za kunadi Kenya machoni pa jumuiya ya kimataifa. 

Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje yupo nchini Uswizi kwa ziara rasmi ya siku tatu.

Akiwa nchini humo, Mudavadi amepangiwa kutoa hotuba katika tukio la ngazi ya juu lenye kaulimbu, “kambi za makazi: vituo vya kijamii na kijamii kwa ujumuishaji wa wakimbizi nchini Kenya” litakalofanyika pembezoni mwa kikao cha 74 cha kamati kuu ya mpango wa kamishna mkuu (Excom 2023).

“Lengo la mkutano wa ngazi ya juu ni kuwezesha washiriki kupata uelewa na utambuzi wa mitazamo ya mabadiliko ya ujumuishaji wa wakimbizi, na wajibu wao katika uhamasishaji wa jamii zenye haki, jumuishi, zenye amani na maendeleo,” inasema taarifa kutoka kwa Ofisi ya Waziri mwenye Mamlaka Makuu.

Mudavadi pia atafanya mkutano wa pande mbili na Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR Filippo Grandi na pia Julieta Noyes ambaye ni Naibu Waziri Msaidizi wa Idadi ya watu, Wakimbizi na Uhamiaji nchini Marekani.

Tangu kuongezewa wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje, Mudavadi amezuru nchi za Uganda na Rwanda na ameapa kutetea maslahi ya Kenya ndani na nje ya nchi.

Website | + posts