Home Habari Kuu Mudavadi atoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za upatikanaji haki

Mudavadi atoa wito wa kuimarishwa kwa juhudi za upatikanaji haki

Mudavadi alidokeza kuwa idara ya Mahakama inajizatiti kuhakikisha wakenya wote wanapata huduma za mahakama.

0

Waziri mwenye mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, ametoa wito idara ya mahakama kushirikiana na taasisi zingine zilizoko katika mfumo wa sheria, kuhakikisha haki inapatikana kwa kila mkenya.

“Narejelea kusema kuwa serikali haitalegea katika kujitolea kwake kuunga mkono idara ya mahakama katika kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kuzingatia sheria na kulinda haki ya wananchi,” alisema Mudavadi.

Mudavadi alisema katiba ya Kenya ya mwaka 2010, imeorodhesha maadili na kanuni zinazopaswa kufuatwa na maafisa wa umma, asasi za serikali na wananchi.

Waziri huyo alisema nafasi ya Kenya miongoni mwa nchini zinazotekeleza demokrasia katika kanda na kimataifa, imetokana na hatua ya kufanyia katiba marekebisho.

“Ni miaka 13 sasa, na tunapaswa kujivunia kwa yale tumetekeleza. Imetuchukua muda mfupi kutekeleza katiba mpya, ikizingatiwa kuwa katika mataifa mengine imechukua muda mrefu na hata kusababisha machafuko,” alidokeza waziri huyo.

Mudavadi aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mkakati wa mageuzi ya kijamii kupitia upatikanaji wa haki wa kati ya mwaka 2023-2033 ambapo pia ripoti ya kila mwaka ya Hali ya utendakazi wa idara ya mahakama na utekelezaji wa haki ya mwaka wa fedha wa 2022-2023 ilitolewa.

Huku akipongeza idara ya mahakama kutokana na jinsi ambavyo imetekeleza majukumu yake, Mudavadi alidokeza kuwa idara hiyo inajizatiti kuhakikisha wakenya wote wanapata huduma za mahakama.