Home Taifa Mudavadi asisitiza umuhimu wa amani kitaifa na kimataifa

Mudavadi asisitiza umuhimu wa amani kitaifa na kimataifa

0
kra

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha amani katika kiwango cha kitaifa, kikanda na kimataifa kwa lengo la kuimarisha usalama wa binadamu wote.

Musalia alikuwa akizungumza katika uwanja wa Uhuru Gardens Nairobi jana Jumapili, Septemba 8, 2024, alipohudhuria tamasha lililoandaliwa na wizara yake la “Harmony4Haiti” ili kuhimiza maelewano kwa ajili ya Haiti.

kra

Alizungumzia jinsi machafuko huvuruga amani na kuongeza migogoro, hali ambayo husababisha ukosefu wa chakula, kutopatikana kwa huduma za afya na elimu na hivyo kuharibu jamii.

Huku akimshukuru Rais William Ruto kwa kuitikia miito ya watu wa Haiti na kusimama nao, Mudavadi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na akaitaka jamii ya kimataifa kuunga Kenya mkono nchini Haiti.

“Ni muhimu tushirikiane na ninaomba jamii ya kimataifa ijiunge na Kenya nchini Haiti kwa kuchangia maafisa zaidi wa polisi au hata pesa ili wanawake, vijana na watu wote wa Haiti wapate amani na ustawi.” alisema Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

Kadhalika, alipongeza maafisa wa polisi wa Kenya kwa kuteuliwa kuongoza operesheni ya kurejesha amani nchini Haiti huku akitambua uadilifu na kujitolea kwao katika operesheni za amani ulimwenguni.

Alimpongeza kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Gilbert Masengeli, Naibu Mshauri wa Usalama Joseph Boinnet na kundi la vijana mabalozi wa amani kwa ujasiri wao wa kutetea amani nchini Haiti.

Mudavadi alikuwa ameandamana na katibu wa masuala ya kigeni Korir Sing’oei, mkuu wa wafanyakazi katika afisi yake Joseph Busiega, mabalozi Beyene Russom wa Eritrea, Luis Levit wa Argentina, William McDonald wa Barbados, Gențiana Șerbu wa Romania na Romy Sonia Tincopa Grados wa Peru.

Website | + posts