Home Habari Kuu Mudavadi ashiriki mazungumzo na Blinken

Mudavadi ashiriki mazungumzo na Blinken

0

Waziri mwenye mamlaka makuu aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, ameshiriki meza ya mazungumzo na mwenzake wa Marekani Antony Blinken na kujadili maswala mbalimbali yanayohusu kanda ya Afrika Mashariki na ulimwengu.

Baadhi ya maswala hayo ni ushirikiano wa kiuchumi, amani, migogoro ya kanda ya Afrika Mashariki na kutatizika kwa mipangilio ya dunia kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati.

Kwenye kauli yake, Mudavadi amesema kuwa, “Mazungumzo baina ya Kenya na Marekani yamelenga upatanisho wa watu na misukosuko ya kiuchumi Afrika Mashariki, vile vile tunashukuru usaidizi wa muda mrefu kwenye maswala ya tabia nchi na vita dhidi ya ugaidi”.

Mudavadi ambaye amekuwa kwenye safari ya siku tatu nchini humo, ameongeza kuwa walijadili swala la kupeleka polisi wa Kenya nchini Haiti na mipango maalum ya kuboresha maisha ya watu wa Haiti.

Wakati huo huo, alidokeza kwamba Blinken amekumbatia ombi la kuwepo kwa mazungumzo ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya Kenya na Marekani (STIP) na pia lile la kuongeza muda wa kipengee cha ukuaji na nafasi ya Afrika cha AGOA.

Alidokeza kuwa juhudi hizi zitafanikisha kupanuka kwa shuguli na usafirishaji usiotozwa ushuru wa bidhaa za Kenya na Afrika.