Home Habari Kuu Mudavadi ahudhuria sherehe za Jamhuri London

Mudavadi ahudhuria sherehe za Jamhuri London

0

Waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi anayezuru Uingereza alihudhuria hafla ya kusherehekea sikukuu ya Jamhuri jijini London.

Kenya inapotimiza miaka 60 tangu ijipatie uhuru, wakenya wanaoishi Uingereza walikongamana katika jumba la Lancaster jijini London kusherehekea.

Kulingana na Mudavadi, chaguo la kuandaa hafla hiyo katika jumba la Lancaster ni muhimu na la kihistoria kwani hapo ndipo mazungumzo kuhusu mfumo wa kikatiba na uhuru yaliandaliwa.

Alisifia wakenya wanaoishi Uingereza akisema wameendelea kudhihirisha moyo wa kipekee wa wakenya unaendelea kukua mbali na nyumbani.

Waziri Mudavadi alishukuru ubalozi wa Kenya jijini London kwa kuandaa hafla hiyo, akiongeza kwamba anajivunia yale ambayo Kenya imetimiza hadi sasa.

Alitaja vikwazo ambavyo nchi hii imekiuka na ahadi ya mambo mazuri siku za usoni.

Kabla ya hafla hiyo, Mudavadi alimzuru
Sir Clive Alderton, katibu wa kibinafsi wa mfalme Charles na malkia Camilla katika kasri la Buckingham jijini London.

Wawili hao walizungumzia ziara iliyofanikiwa pakubwa ya mfalme Charles nchini Kenya, jukumu la jumuiya ya madola katika masuala mbali mbali ya ulimwengu na maandalizi ya mkutano ujao wa viongozi wa nchi za jumuiya hiyo mwaka ujao nchini Samoa.

Sir Clive alishukuru Rais William Ruto kwa kuwa mwenyeji bora wa mfalme wakati wa ziara yake nchini na uongozi wake katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi.