Home Kimataifa Mudavadi ahimiza KRA kuimarisha juhudi za ukusanyaji ushuru

Mudavadi ahimiza KRA kuimarisha juhudi za ukusanyaji ushuru

Takwimu za hivi majuzi zinaashiria kuwa KRA imedumisha ongezeko la ukusanyaji ushuru, baada ya kukumbatia mfumo bora wa kibiashara wa kukusanya ushuru.

0
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.
kra

Halmashauri ya Ukusanyaji  Ushuru   nchini  (KRA) imehimizwa kuwatia moyo walipa ushuru  kama sehemu ya kuwachochea kutoa ushuru  kwa hiari.

Waziri mwenye mamlakaa makuu,  Musalia Mudavadi amesema serikali imeanzisha hatua kabambe za mageuzi  kwenye usimamizi wa ushuru ili kufikia uwezo kamili wa kukusanya ushuru.

kra

Alidokeza kuwa KRA inafaa kukumbatia utendaji kazi wa kitaalam  na kuongeza ufanisi na usawa inapotekeleza majukumu yake. Alisema  halmashauri hiyo lazima wakati wote ihakikishe uwajibikaji na uwazi ili serikali kufikia malengo yake katika ukusanyaji wa ushuru.

“Mataifa yote hutegemea ushuru katika utoaji huduma kwa umma na kuhakikisha ukuaji wa uchumi. Kupitia ushuru tunajenga hospitali, shule, tunalipa walimu, tunajenga mitandao mizuri ya barabara na kutoa huduma za usalama miongoni mwa huduma zingine za umma,” alisema Mudavadi.

Mudavadi alikuwa akizungumza mjini Eldoret wakati wa kufuzu kwa maafisa wa Halmashauri hiyo  katika chuo cha kutoa  mafunzo  kwa wafanyakazi wa halmashauri hiyo, ambako alimwakilisha Rais William Ruto.

Takwimu za hivi majuzi zinaashiria kuwa KRA imedumisha ongezeko la ukusanyaji ushuru, baada ya kukumbatia mfumo bora wa kibiashara wa kukusanya ushuru.

KRA ilinakili ukuaji wa ukusanyaji ushuru wa asilimia 6.7 katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 baada ya kukusanya shilingi trilioni 2.166, ikilinganishwa na shilingi trilioni 2.031 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha wa mwaka 2021/2022.

Website | + posts