Home Kaunti Muda wa ushirikiano wa Red Cross na serikali ya kaunti ya Bomet...

Muda wa ushirikiano wa Red Cross na serikali ya kaunti ya Bomet waongezwa

0

Serikali ya kaunti ya Bomet na shirika la msalaba mwekundu nchini zimetia saini mkataba wa maelewano ili kuongeza muda wa ushirikiano kati yao kwa muda wa mwaka mmoja zaidi.

Katibu mkuu wa shirika la msalaba mwekundu Dkt. Ahmed Idris na Gavana Profesa Hillary Barchok, walitia saini mkataba huo katika afisi ya Gavana mjini Bomet leo kwa lengo la kutoa fursa ya kukamilishwa kwa awamu ya pili ya mpango wa pamoja wa maendeleo unaodhamiriwa kuboresha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo.

Mpango huo wa maendeleo unaangazia upatikanaji wa chakula, maji na usafi, afya na lishe bora, mazingira na ulinzi dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Gavana Barchok anasema amefurahia kutia saini mkataba huo wa maelewano.

Kabla ya hapo, Gavana Barchok na kundi lake na Daktari Idriss na kundi lake walizuru mradi wa kituo cha afya cha mama na mtoto kujifahamisha na anasema umekamilika kwa kiwango cha asilimia 90.

Kitakapokamilika, kituo hicho kitapunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya rufaa ya Longisa.

Ushirikiano huo kati ya serikali ya kaunti ya Bomet na shirika la msalaba mwekundu umekuwepo kwa muda wa miaka 10 sasa.