Home Habari Kuu Mtu mwingine afariki kutokana na mkasa wa gesi Embakasi

Mtu mwingine afariki kutokana na mkasa wa gesi Embakasi

0
Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura.

Mtu mmoja zaidi amefariki kutokana na mkasa wa mlipuko wa gesi uliotokea wiki jana katika eneo la Embakasi kaunti ya Nairobi.

Hii inafikisha saba, idadi jumla ya watu ambao wamefariki kutokana na mkasa huo kufikia sasa.

Kupitia kwa taarifa msemaji wa serikali Isaac Mwaura alitangaza pia kukamatwa kwa Linet Cheruiyot, afisa mkuu wa mazingira katika shirika la kitaifa la utunzanji wa mazingira NEMA.

Cheruiyot anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Embakasi na alitarajiwa kufikishwa katika mahakama ya Makadara leo alasiri.

Watu ambao wamekamatwa kuhusiana na mkasa huo kufikia sasa ni watano ambapo wanne kati yao walifikishwa mahakamani jana.

Mfanyibiashara Derrick Kimathi alifikishwa katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi ambapo waendesha mashtaka waliomba siku 21 ili kukamilisha uchunguzi.

Kimathi alikuwa ameandamana na maafisa wa shirka la NEMA ambao ni David Ongare mkurugenzi wa kufuata masharti ya kimazingira , Joseph Makau msimamizi wa kitengo cha kukadiria athari kwa mazingira na Mirriam Kioko.

Walishtakiwa kwa tuhuma za mauaji na kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill jijini Nairobi.

Mwaura alisema pia kwenye ripoti hiyo kwamba wahasiriwa wote ambao walikuwa wanahifadhiwa katika ukumbi wa jamii wa Embakasi wameondoka.

Wamepatiwa makazi mbadala na wengine wanaishi na ndugu jamaa na marafiki.