Mtu mmoja amethibitishwa kufariki huku wengine watano wakiwa hawajulikani waliko baada ya mashua waliosafiria kuzama katika ziwa Baringo kaunti ya Baringo.
Akithibitisha kisa hicho, kamanda wa polisi kaunti ya Baringo Julius Kiragu alisema waumini 23 hasa vijana kutoka kanisa la Revival, walikuwa wakielekea kisiwa cha Kokwa katika ziwa hilo kutoka kata za Salabani.
Kiragu alieleza kuwa walipokuwa wakiendelea na safari, mashua iliyokuwa imebeba watu kupita kiasi ilizama.
Alisema watu 17 waliokolewa na juhudi za kuwatafuta wengine watano zingali zinaendelea.
Kiragu aliongeza kuwa mashua hiyo ilishindwa kuendelea na safari kutokana na mawimbi yenye nguvu katika ziwa hilo.
Naibu Gavana wa kaunti ya Baringo Felix Maiyo, aliyefika katika eneo la mkasa, aliwataka wanaotumia safari za majini, kuwa waangalifu zaidi.