Home Habari Kuu Mtu mmoja afariki, nyumba kadhaa zachomwa katika shambulizi la kigaidi Lamu

Mtu mmoja afariki, nyumba kadhaa zachomwa katika shambulizi la kigaidi Lamu

0

Mtu mmoja aliaga dunia na nyumba kadhaa kuchomwa katika shambulizi la kigaidi linaloshukiwa kutekelezwa macheo na wanamgambo wa Al-Shabaab katika kijiji cha Witho, kata ya Salama katika kaunti ya Lamu. 

Kwa mujibu wa wakazi, wanamgambo hao walivamia makazi yao na kuiba ng’ombe na nafaka miongoni mwa vyakula vingine.

Mashambulizi ya hapa na pale yameripotiwa kaunti ya Lamu katika siku za hivi karibuni na nyakati nyingine kusababisha vifo vya watu kadhaa na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa.

Wakazi sasa wanatoa wito kwa serikali kuchukua hatua kali za kukomesha mashambulizi ya kigaidi katika eneo hilo na katika vijiji jirani. Wanasema wanaishi kwa hofu tangu kuanza kwa mashambulizi katika eneo hilo mapema mwaka huu.

Wakazi walitoa wito huo wakati ambapo serikali imesema itatuma vikosi maalum kaskazini mwa nchi na maeneo ya juu ya Pwani zikiwemo kaunti za Lamu na Tana River kwa kusudi la  kukabiliana vilivyo na magaidi wanaowahangaisha raia.

“Ili kukabiliana ipasavyo na tishio la ugaidi na itikadi kali, serikali inavipeleka vikosi maalum kaskazini mwa nchi na maeneo ya juu ya Pwani zikiwemo kaunti za Tana River na Lamu ili kupambana vikali na kuwaangamiza wahalifu wanaowahangaisha wakazi wasiokuwa na hatia,” amesema Waziri wa Usalama wa Kitaifa Kithure Kindiki.

“Serikali itaendelea kuwapatia maafisa wetu silaha za kisasa na teknolojia ili kuongeza uwezo wao wa kukabiliana na wahalifu.”

Kindiki aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa usalama ulioandaliwa katika eneo la Wayu, kaunti ndogo ya Galledyertu, kaunti ya Tana River akiandamana na Gavana wa kaunti hiyo Godhana Dhadho na Seneta Danson Mungatana miongoni mwa viongozi wengine.

Website | + posts