Aliyekuwa mtangazaji nguli wa habari za michezo nchini Kenya Peter Kimeu ameaga dunia, baada ya kuhudumia shirika la utangazaji nchini, KBC kwa miaka 33.
Akiwa katika shirika la KBC, Kimeu alitayarisha na kusimulia vipindi maarufu vya michezo katika idhaa ya taifa enzi hizo, vikiwemo Ulimwengu wa Michezo kila siku na Ukumbi wa Spoti kila Jumamosi na kipindi kilichonoga zaidi cha Salamu za Vijana.
Kimeu alistaafu mwaka 2022 baada ya kuhudumu kwa miaka 33.
Ustadh Peter Kimeu aliyejiunga na KBC mwaka 1989, aliripotiwa kufariki jana Jumapili.
Baadhi ya ufanisi wake mkubwa ulikuwa kuwalea chipukizi na aliacha historia ya kuwafunza na kuwakuza watangazaji mashuhuri katika kitengo cha michezo kama vile Vereso Mwanga, Bonnie Musambi, Vincent Ateya, Jerida Andayi, Fred Nyongesa Ongalo, Mary Wavinya Musa na wengine tumbi nzima.
Kwa kawaida, Mzee Kimeu Nathan alikuwa mwenye busara, maarifa na hakupenda kamwe mafarakano kazini.
Nilipata fursa adimu ya kuwa mwanafunzi wake nikiwa katika masomo ya nyanjani KBC kuanzia mwaka 2009, na alinifunza uandishi bomba wa taarifa za michezo na utangazaji kando na uchanganuzi, kikubwa alichoniambia nyakati zote umuhimu wa kufanya utafiti kabla ya kuenda hewani na kujiamini ukiwa nyuma ya bomba.
Kwa maisha ya kawaida, Kimeu alikuwa mcheshi na mwenye bashasha.
Kimeu alitangaza mashindano makuu kama vile mbio za nyika ulimwenguni ziliazoandaliwa Mombasa mwaka 2007, mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini, michauno ya kombe la mataifa ya Afrika na ile ya CECEFA.
Kimeu amemuacha mjane na watoto wawili wa kiume.
Kutoka jamii ya KBC, makiwa kwa familia ya Gwiji Kimeu.