Baraza la Mawaziri limeidhinisha mswada wa marekebisho wa ukaguzi wa mahesabu wa umma wa mwaka 2023, ambao unaboresha uhuru wa mkaguzi mkuu wa Mahesabu.
Mswada huo pia unaimarisha uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya rasilimali za umma.
Pia unampa mamlaka mkaguzi mkuu wa mahesabu ya Serikali kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa uwajibikaji wa wananchi ili kuhakikisha ushiriki wa umma katika ukaguzi huo.
Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali pia atakuwa na mamlaka ya kufanya ukaguzi wa uzingatiaji ili kuchunguza iwapo shirika la umma limezingatia sheria husika katika usimamizi wa rasilimali za umma.
Katika azma ya kuimarisha ubora wa maisha ya wananchi, baraza la mawaziri pia liliidhinisha sera ya taifa ya mafao ya kustaafu.
Sera hiyo itaoanisha utawala, kupanua wigo wa sekta isiyo rasmi, kuhakikisha utekelezaji, uwezo wa kumudu na utoshelevu wa manufaa kando na kuanzisha manufaa ya matibabu baada ya kustaafu.
Aidha, Baraza la Mawaziri liliidhinisha maandalizi ya kuandaa Kongamano la Vijana la Connekt Africa 2023 lililopangwa kufanyika Nairobi Desemba hii.
Mpango huo ambao umeidhinishwa na Umoja wa Afrika unalenga kuwawezesha vijana kupitia ujasiriamali, uvumbuzi na uongozi.
Katika kile ambacho kinaweza kuongeza ukuaji na uundaji wa ajira, Baraza la Mawaziri liliidhinisha zaidi sera, programu na miradi kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.
Katika kuunga mkono uundaji bora wa nafasi za kazi na ukuaji wa biashara ndogo ndogo, Baraza la Mawaziri liliidhinisha Mradi wa Mabadiliko ya Ajira na Uchumi nchini Kenya.
Pia liliidhinisha Mpango wa Usafi wa Mazingira na Usafi wa Maji wa Kenya, ambao unalenga kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira, kukomesha kwenda haja kubwa mahali pasipo stahili, na kuimarisha uwezo wa kifedha wa watoa huduma za maji.