Home Habari Kuu Mswada wa kumtimua Gavana Mwangaza kuwasilishwa Jumanne

Mswada wa kumtimua Gavana Mwangaza kuwasilishwa Jumanne

Mwangaza amekuwa akishtumiwa kwa kumpiga kumbo naibu wake Isaac Mutuma, katika kuendesha shughuli za kaunti hiyo.

0

Kwa mara nyingine, Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza yupo mashakani.

Awali, alinusurika makali ya Wawakilishi Wadi kumtimua afisini baada ya bunge la Seneti kupuuzilia mbali madai aliyolimbikiziwa.

Miezi kadhaa baada ya utulivu kiasi kushuhudiwa tangu Mwangaza kukwepa shoka la kumtimua, Wawakilishi Wadi wamechacha tena.

Kiasi kwamba leo Jumanne, mswada mwingine wa kumtimua Gavana Mwangaza utawasilishwa katika bunge la kaunti hiyo wakati wa kikao cha asubuhi.

Imekuwa kawaida kama ibada kwa Gavana Mwangaza kulumbana na Wawakilishi Wadi wa kaunti hiyo.

Mwangaza amekuwa akishtumiwa kwa kumpiga kumbo naibu wake Isaac Mutuma katika kuendesha shughuli za kaunti hiyo.

Mutuma amemshutumu Gavana Mwangaza kwa kumzuia kuhudhuria mikutano ya mawaziri wa kaunti hiyo na kutofadhili afisi yake na hivyo kuhujumu utendakazi wake.

Aidha hivi maajuzi, Gavana huyo alimwandikia barua Spika wa Seneti Amason Kingi akiitaka Kamati ya Seneti inayoshughulikia Masuala ya Ugatuzi kuchukua jukumu la kusuluhisha mtafaruku kati ya pande hizo mbili, ambao kwa muda mrefu umeathiri utoaji huduma katika kaunti hiyo.

“Naandika kukuarifu mzozo uliotokota ambao serikali yangu inakabiliana nao,” ilisema barua hiyo ya Gavana Mwangaza.

Kulingana naye, aliridhiana na Wawakilishi Wadi baada ya jaribio lao la awali la kumtimua afisini kugonga mwamba, lakini katika siku za hivi maajuzi, tofauti kati yao zimechipuka tena.

Katika barua hiyo, Gavana Mwangaza alisema hana Wawakilishi Wadi mahususi wanaomuunga mkono kwani alichaguliwa kwenye wadhifa huo kama mgombeaji huru.

Katika kipindi ambacho amehudumu, anasema amekuwa akiwategemea Wawakilishi Wadi wa chama tawala cha UDA, lakini chama kimewaelekeza kutomuunga mkono kamwe.

Anawanyoshea kidole cha lawama Naibu wake Isaac Mutuma, Seneta wa Meru Murungi Kathuri, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na wabunge kutoka kaunti hiyo anaosema wamekula njama ya kumhujumu.

Website | + posts