Mamlaka ya barabara kuu nchini, KENHA imewahimiza madereva kujiepusha na kubeba mizigo kupita kiasi kwani hatua hiyo inachangia pakubwa uharibufu wa barabara humu nchini.
Akizungumza katika kituo cha kupimia uzani cha Mlolongo, Naibu Mkurugenzi wa vituo vya kupimia uzani vya mamlaka hiyo Michael Ngala amesema watakaopatikana wakipakia mizigo kupita kiasi watatozwa faini kwa mujibu wa sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Amesema hatua hiyo inalenga kuwaogofya madereva kutofanya hivyo ili kuzuia uharibifu wa barabara kuu.
Aidha amesema wamewaimiza watumizi wa barabara na washikadau wa uchukuzi kuzingatia sheria.
Idadi ya malori yanayopita kwenye kituo hicho ni 16,000 kwa siku.
Kulingana na afisa huyo, magari ya wanaopatikana kubebea uzani kupita kiasi huzuiliwa kwenye kituo hicho na kupewa muda wa siku tatu kulipia ada wanazotozwa, na wasipowajibika wanalazimika kulipia ada ya maegesho ya dola 50 kwa siku.