Home Kimataifa Mshindi wa Tuzo ya Nobel ahukumiwa kifungo jela

Mshindi wa Tuzo ya Nobel ahukumiwa kifungo jela

0

Mahakama nchini Bangladesh imemhukumu mshindi wa tuzo ya Nobel Muhammad Yunus kifungo cha miezi sita jela kwa kukiuka sheria za kazi za nchi hiyo.

Wafuasi wa Profesa Yunus wanasema kesi hiyo imechochewa kisiasa.

Mchumi huyo maarufu na wenzake watatu kutoka kampuni yao ya Grameen Telecom – walipatikana na hatia ya kushindwa kuunda mfuko wa ustawi wa wafanyakazi wao.

Wote wanne wanakana kufanya makosa yoyote na wamepewa dhamana wakisubiri rufaa.

“Kama mawakili wangu walivyoeleza mahakamani, hukumu hii dhidi yangu ni kinyume cha sheria na haingii akilini,” Prof Yunus alisema katika taarifa iliyotolewa baada ya hukumu hiyo.

Yunus mwenye umri wa miaka 83, anayejulikana kimataifa kwa kitabu chake “banker to the poor,” anasifiwa kwa kuwa muasisi wa mfumo wa mikopo midogo midogo inayosaidia kuondoa mamilioni ya watu kwenye umaskini.

Prof Yunus na Benki yake ya Grameen walitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi hiyo mwaka wa 2006.