Taifa la Kenya kwa mara nyingine limegubikwa na biwi la simanzi kufuatia kifo cha mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji na mita 5,000 Henry Rono mapema Alhamisi.
Rono amefariki akipokea matibabu katika Hospitali ya Nairobi South akiwa na umri wa miaka 72.
Rono alizaliwa katika kijiji cha Kaptabagon, kaunti ya Nandi mnamo Februari 12 mwaka 1952.
Shirikisho la riadha Kenya (AK) limetangaza kifo chake kupitia taarifa kwa vyombo vya habari likisema kuwa mwanariadha hiyo alifariki Alhamisi asubuhi baada ya kulazwa kwa siku kumi.
“Shirikisho la riadha Kenya (AK) linatangazia umma kwa masikitiko kifo cha mwanariadha wa zamani Bw Henry Rono kilichotokea leo saa nne na nusu asubuhi. Alikuwa amelazwa katika hospitali ya Nairobi South kwa siku kumi zilizopita,” imesema AK kupitia ujumbe.
Rono alishiriki mbio za mita 3,000, mita 3,000 kuruka viunzi na maji, mita 5,000 na mita 10,000.
mjini Edmonton nchini Canada, akinyakua nishani za dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Baadaye mwaka huo kwenye michezo ya Afrika mjini Algiers nchini Algeria, Rono alinyakua nishani za dhahabu katika mbio za mita 10,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Rono atakumbukwa kwa kuvunja rekodi nne za dunia za mbio za mita 10,000, mita 5,000, mita 3,000 na mita 3,000 kuruka viunzi na maji.
Rono alihamia nchini Marekani hadi mwaka wa 2019 aliporejea nchini.
Mwanariadha huyo alikosa kushiriki michezo ya Olimpiki baada ya Kenya kususia makala ya mwaka 1976 na 1780.
Kifo cha Rono kimetokea siku nne baada ya mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za Marathon Kelvin Kiptum kuaga dunia kwenye ajali ya barabara pamoja na kocha wake raia wa Rwanda Gervais Hakizimana Jumapili usiku eneo la Kaptagat, kaunti ya Elgeyo Marakwet