Home Habari Kuu Msemaji wa serikali atetea safari za Rais nje ya nchi

Msemaji wa serikali atetea safari za Rais nje ya nchi

0

Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ametoa hotuba yake ya kwanza kikazi tangu alipoteuliwa kuhudumu kwenye wadhifa huo na alifungua na utetezi wa safari za Rais William Ruto nje ya nchi.

Sera ya kigeni ya Kenya, alisema imesimikwa kwenye maono ya Kenya yenye amani, yenye mafanikio na yenye ushindani na azimio la kubashiri, kukuza na kulinda maslahi ya Kenya na mwonekano wake ulimwenguni.

Alisema hayo yanaweza kuafikiwa kupitia dimplomasia bunifu na kuchangia juhudi za kuhakikisha dunia iliyo na haki, amani na usawa.

Kulingana na Mwaura, Rais William Ruto amefanya safari 39 nje ya nchi tangu alipoingia mamlakani yapata mwaka mmoja uliopita na amekuwa mwenyeji wa marais na viongozi wa nchi wapatao 30.

Alitetea safari hizo akisema Rais ndiye mjumbe mkuu wa nchi hii ughaibuni na kushughulikia masuala ya kigeni ni mojawapo ya majukumu yake kupitia kwa mamlaka aliyopatiwa kuongoza taifa.

Ziara hizo za nje pamoja na ujio wa viongozi wa nchi nyingine Kenya zimesababisha kuafikiwa kwa mikataba mbali mbali ambayo inadhihirisha uwezo mkubwa wa Kenya katika diplomasia.

Msemaji Mwaura aliorodhesha baadhi ya faida zilizopatikana kutoka kwa safari za kikazi za Rais William Ruto ambazo zilitokana na mikataba ya maelewano kama vile fursa 350,000 za ajira kwa wakenya huko Saudi Arabia na uwekezaji katika kawi safi.

Alitaja pia Mikataba ya uwekezaji wa thamani ya Pauni bilioni 5 nchini Kenya iliyoafikiwa kwenye mazungumzo na waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na ufunguzi rasmi wa ubalozi wa Kenya nchini Senegal.

Mwaura alitaja pia mkataba wa kuidhinisha mtandao mmoja wa mawasiliano ya simu za rununu Afrika Mashariki ulioafikiwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda kati ya mikata mingine mingi.

Kuhusu upanzi wa miti na juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, msemaji wa serikali alisema kwamba mpango huo uliafikia upanzi wa miche milioni 150 kwenye siku iliyotengwa ya Jumatatu Novemba 13, pekee.

Alisema serikali ya Kenya kwanza inajibidiisha kupunguza gharama ya maisha ili wakenya waweze kuishi maisha mazuri.

Website | + posts