Home Habari Kuu Msajili wa vyama vya kisiasa alalamikia kupunguzwa kwa fedha za vyama vya...

Msajili wa vyama vya kisiasa alalamikia kupunguzwa kwa fedha za vyama vya kisiasa

0

Msajili wa vyama vya kisiasa nchini Anne Nderitu amelalamikia hatua ya serikali ya kupunguza mgao wa fedha zinazotengewa vyama vya kisiasa kwenye bajeti.

Akizungumza katika kikao na kamati ya bunge la taifa kuhusu haki na masuala ya kisheria, Nderitu alielezea kwamba kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024, pesa za vyama zimepunguzwa kutoka bilioni 1.475 hadi shilingi milioni 608.

Kulingana naye, tangu hazina ya vyama vya kisiasa ilipobuniwa, serikali haijakuwa ikitimiza mahitaji ya kifungo nambari 24 sehemu ya kwanza (a) ya sheria ya vyama vya kisiasa.

Nderitu alikuwa amealikwa na kamati hiyo iliyo chini ya uenyekiti wa George Gitonga Murugara kuelezea kuhusu usimamizi wa pesa za hazina ya vyama vya kisiasa.

Alisema kwamba afisi yake imeandikia wizara ya fedha kutaka maelekezo kuhusu jinsi ya kugawa pesa hizo na wanasubiri majibu.

“Kwa sababu Kenya ni nchi ya vyama vingi, afisi hii inatambua kwamba vyama ni muhimu kwa kuendeleza usimamizi bora na uhuru wa kuchagua na vinahitaji ufadhili kuendesha shughuli zake.” alisema Nderitu.

Aliomba bunge lisaidie katika ugawaji wa fedha za hazina ya vyama vya kisiasa na wabunge waunge mkono uhuru wa kiuchaguzi nchini.

Mwenyekiti Murugara alikubaliana na Nderitu kwamba vyama vinahitaji fedha za kutosha kuendesha shughuli zao huku akielezea kwamba kinachosababisha kupunguzwa kwa migao katika bajeti ni ukosefu wa fedha.

Aliahidi kwamba malalamishi ya afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa yatajumuishwa kwenye ripoti ya kamati hiyo ya haki na sheria.

Website | + posts