Home Burudani Msafara wa kusaka talanta Nairobi wazinduliwa

Msafara wa kusaka talanta Nairobi wazinduliwa

0

Msafara wa kusaka talanta katika maeneo mbali mbali ya kaunti ya Nairobi kwa jina “Kipaji 47 Caravan” umezinduliwa.

Mwanachama wa kamati kuu ya kaunti ya Nairobi anayehusika na masuala ya ushirikishi wa umma na huduma kwa wateja Daktari Anastasia Nyalita ndiye alizindua msafara huo.

Msafara huo utapitia kwenye wadi zote za kaunti ya Nairobi, kusaka na kutambua walio na talanta mbali mbali ambao watahusishwa kwenye tamasha ya Nairobi.

Watakaochaguliwa kutoka mitaani, watapelekwa kwenye kambi ya maandalizi kwa ajili ya tamasha hiyo ambayo imepangiwa kuandaliwa Disemba 12 hadi 17, 2024 katika bustani ya Uhuru.

Awali serikali ya kaunti ya Nairobi ilikuwa imetoa mwaliko kwa wenye talanta ambao wangependa kushirikishwa kwenye tamasha hiyo kutuma video za dakika moja wakionyesha vipaji vyao kupitia mtandao wa Whatsapp.

Umri wa washiriki ni kati ya miaka 18 na 80 na walemavu wamehimizwa kushiriki.