Mwigizaji wa filamu za Nigeria almaarufu Nollywood John Okafor amefariki akiwa na umri wa miaka 62. Anasemekana kuaga dunia Jumamosi Machi 2, 2024 katika hospitali moja nchini Nigeria.
Okafor ambaye anafahamika sana kama Mr. Ibu alianza kuugua Oktoba 2023, wakati ambapo familia yake iliomba usaidizi wa kifedha kugharamia matibabu.
Mwezi mmoja baadaye ilitangazwa kwamba mguu wake mmoja ulikatwa kama njia ya kuokoa maisha yake. Mishipa ya damu kwenye mguu huo ilikuwa imedhurika suala ambalo halikugunduliwa mapema na madaktari.
Watu wengi maarufu nchini Nigeria wamemwomboleza marehemu Okafor kupitia mitandao ya kijamii. Mama Patience Ozokwor maarufu kama Mama G alinukuu kifungu cha Biblia 1 Wakorintho 15:55 ambacho kinasema “Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”
Mercy Johnson Okojie aliandika, “Ni salama … Pumzika kwa amani…” naye Ruth Kadiri akaandika “Lala salama baba.”.