Juhudi za Jaji Mkuu Martha Koome za kuimarisha upatikanaji wa haki hasa kwa waliotengwa katika jamii zimefika katika mji wa Kakuma, mji ambao unahusishwa na wakimbizi.
Koome alizindua kituo mbadala cha kupata haki mjini humo pamoja na mfumo wa kuweka kesi kwa njia ya kielektroniki Jumanne, Agosti 29, 2023.
Akizungumza katika mahakama ya Kakuma, Jaji Mkuu alisifia kujitolea kwa wakazi wa mji huo wa Kakuma kukaribisha na kukumbatia wakimbizi ambao mara nyingi wako katika hatari ya kuathirika.
Jaji Mkuu alisisitiza kwamba idara ya mahakama imejitolea kuhakikisha mahakama zinahudumia wenyeji na hata wakimbizi huku akiwaomba waendelee kuishi kwa amani na umoja.
“Mizozo inapotokea, ninawaomba mtumie mbinu za utatuzi za mahakama na kituo mbadala cha haki ili kuhakikisha mizozo hiyo inatatuliwa haraka,” Koome aliambia wakazi wa Kakuma.
Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi alisema kwamba uzinduzi wa vituo mbadala vya kupata haki utaimarisha upatikanaji wa haki kwa jamii hiyo ambayo kwa miaka mingi imeorodheshwa chini ya waliotengwa nchini Kenya.
Wakili Stephen Mogaka ambaye pia ni mbunge wa eneo la Mugirango Magharibi katika kaunti ya Nyamira aliyewakilisha mwenyekiti wa kamati ya haki katika bunge alisema kifungu nambari 48 cha katiba kinaelekeza kwamba kila Mkenya awezeshwe kuafikia haki.
Alisema uzinduzi wa leo mjini Kakuma ni hatua muhimu katika kuafikia ahadi hiyo ya katiba kwa kuanzisha mfumo unaokumbatia teknolojia na hivyo kuondoa vizingiti vya kijiografia.
Jaji Koome aliahidi kuzindua mahakama zingine katika maeneo ya Lokichar na Lokitaung, kufuatia ombi la viongozi wa kaunti ya Turkana wakiongozwa na naibu gavana Dkt. John Erus.