Bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 Mary Moraa analenga kutwaa dhahabu katika mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika jijini Paris, Ufaransa mwezi Agosti mwaka huu.
Katika mahojiano ya kipekee na KBC, Moraa aliahidi kujitahidi na kukimbia kwa muda wa kasi wa dakika 1 na sekunde 55 au dakika 1 na sekunde 54, kama mojawapo ya maandlizi yake kwa Olimpiki.
“Lengo langu la kwanza, nataka kuongeza kasi yangu kutoka dakika 1 na sekunde 56 hadi muda wa dakika 1 na sekunde 54 au dakika 1 na sekunde 55,” alisema Moraa.
“Matarajio ni mengi ya Olimpiki hasa kutoka kwa kila mtu baada ya kushinda dhahabu ya dunia mwaka jana, kile tu naweza kusema mambo yakiniendea shwari, nataka nipate dhahabu au nishani ya fedha katika Olimpiki.”
Moraa analenga kuwa mwanamke wa pili wa Kenya kunyakua dhahabu ya Olimpiki baada ya Pamela Jelimo mwaka 2008 mjini Beijing, China.
Washindi wengine wa nishani za Olimpiki katika shindano hilo la mizunguko miwili kwa vipusa ni Janeth Jepkosgei aliyeshinda medali ya fedha mwaka 2008 na Margaret Wambui aliyeshinda shaba mwaka 2016.