Home Kimataifa Mmoja wa wanafunzi wa Tanzania walioshikwa mateka Israel amefariki

Mmoja wa wanafunzi wa Tanzania walioshikwa mateka Israel amefariki

0

Mmoja kati ya wanafunzi wawili wa Tanzania waliotekwa na wapiganaji wa Hamas wakati wa uvamizi wao Israel, amefariki.

Kulingana na taarifa kutoka kwa serikali ya Tanzania iliyotumwa katika vyombo vya habari,  Clemence Felix Mtenga, alikua hajulikani alipo tangu uvamzi wa wapiganaji wa Hamas nchini Israel mnamo tarehe saba mwezi Oktoba 2023.

Marehemu alikuwa miongoni mwa vijana 260 wa Tanzania waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Israel.

Kulingana na taarifa hiyo iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano , tayari serikali imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa marehemu kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati.

Vilevile serikali ya Tanzania kupitia taarifa hiyo imesema kwamba inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwengine kwa jina Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu mashambulizi hayo.

Aidha imewahakikishia raia wake wanaoishi katika mataifa ya kigeni ikiwemo wanafunzo waliopo katika masomo nchini Israel kuwa kupitia ubalozi wake uliopo mjini Tel Aviv , nchini Israel, itaendelea kuwasiliana na mamlaka ya taifa hilo kuhakikisha kuwa Watanzania wote waliopo nchini humo wako salama .