Home Taifa Mlongo aahidi kurejesha Linda Mama iwapo uteuzi wake utaidhinishwa

Mlongo aahidi kurejesha Linda Mama iwapo uteuzi wake utaidhinishwa

0
kra

Daktari Debra Mlongo Barasa aliyeteuliwa na Rais William Ruto kama waziri wa Afya ameahidi kurejesha mpango wa Linda Mama iwapo uteuzi wake utaidhinishwa.

Akizungumza mbele ya kamati ya bunge kuhusu uteuzi wakati wa usaili, Barasa alisema yeye ni mtetezi wa mpango huo na moja kati ya vitu anavyopanga kujumuisha kwenye bima ya afya ya jamii, SHIF.

kra

Mlongo alifafanua kwamba yeye ni mmoja wa walionufaika na mpango huo wa Linda Mama na kwamba kizingiti kikuu cha mpango huo ni ukosefu wa sera za kuongoza mpito.

Mpango wa Linda Mama ulianzishwa na Rais Uhuru Kenyatta mwezi Juni mwaka 2013 kwa lengo la kuondolea kina mama wajawazito mzigo wa kulipia huduma za kujifungua na matibabu kwa watoto wanaozaliwa.

Kina mama hao walihitajika tu kujisajili na kupatiwa kadi maalum na kisha kupokea huduma bila malipo.

Kuhusu tatizo sugu la migomo ya madaktari na wahudumu wengine wa sekta ya afya nchini, Barasa alisema atahakikisha kwamba anashirikiana na vyama vya wahudumu wa afya kuhakikisha migomo inakwisha.

Alipoulizwa kuhusu jinsi atakabiliana na mianya iliyopo na changamoto za kutekeleza bima mpya ya afya ya SHIF, Barasa ambaye alikuwa wa pili kusailiwa, alisema atahusisha mashauriano.

Kulingana naye, ni muhimu kuwaleta wadau wote wa mpango huo pamoja kwa mashauriano kando na kuhamasisha umma kuhusu mpango mzima wa SHIF ili wauchukulie kuwa mpango wao.

Mteule huyo wa wadhifa wa Waziri wa Afya aliahidi pia kufanya utathmini kamili wa pesa zinazosemekana kupotea kutoka kwa Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya, NHIF kabla ya kuchukua hatua.

Website | + posts