Home Kimataifa Mlipuko wapasua barabara jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini

Mlipuko wapasua barabara jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini

0

Mtu mmoja alipoteza maisha na wengine zaidi ya 40 kuachwa na majeraha baada ya kile kinachoshukiwa kuwa mlipuko wa gesi kutokea kwenye eneo moja jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Kiini cha mlipuko huo hakikutambulika mara moja.

Mwili wa mtu huyo ulipatikana usiku wakati maafisa walikuwa wakipekua eneo la mkasa huku kampuni inayosambaza gesi katika eneo hilo ikikanusha uwezekano wa mabomba yake kusababisha mlipuko huo.

Awali walioshuhidia tukio hilo walilichukulia kuwa tetemeko la ardhi lakini kauli hiyo ikakanushwa na wataalamu kwani sehemu za karibu hazikuathirika sana.

Usimamizi wa jiji la Johannesburg umeleta kundi la wataalamu kuchunguza kilichosababisha mlipuko huo ambao ulipasua barabara za Bree na Simmonds ambapo mianya mikubwa ilijitokeza na magari yaliyokuwa yameegeshwa yakaingia humo huku mengine yakiangukia upande.

Kiongozi wa serikali ya mkoa wa Guateng Panyaza Lesufi anasema lengo la uchunguzi huo ni kufahamu kiini cha mkasa huo na kuona iwapo kuna tishio jingine la mkasa sawia ili wachukue hatua za kuuzuia.

Alisema yamkini watu 12 bado wamelazwa kwenye hospitali mbali mbali za jiji hilo kutokana na majeraha waliyopata jana kwenye mkasa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here