Mkuu wa kitengo cha upelelezi nchini, DCI Mohamed Amin amezuru maafisa wa kitengo hicho ambao walijeruhiwa jana Jumapili usiku kwenye makabiliano na mshukiwa katika eneo la Kasarani, Nairobi.
Maafisa hao watatu wamelazwa katika Nairobi Hospital.
Walikuwa wanatekeleza operesheni dhidi ya mshukiwa huyo wa ujambazi katika makazi yake ambapo aliamua kutumia familia yake kama ngao na kusababisha maafisa wa DCI kutofyatua risasi kwa hofu ya kudhuru wanafamilia.
Suala hilo lilisababisha mshukiwa apate fursa ya kufyatua risasi kadhaa ambazo ziliumiza maafisa hao lakini baadaye aliuawa na bunduki yake ikatwaliwa.
Mshukiwa huyo ni mmoja kati ya wengine ambao walikabiliwa na maafisa wa usalama Septemba 14, 2023 huko Kisii ambapo watatu waliuawa.
Amin ameelezea kwamba mshukiwa mwingine alihepa katika tukio la jana na wanamsaka.
Mnamo mwezi Septemba, majambazi hao ambao walikuwa wakisafiri kwenye pikipiki walifuatwa na maafisa wa usalama kutoka kaunti ya Migori hadi kaunti ya Kisii ambapo walifyatuliana risasi na polisi.
Bunduki aina ya AK47 ilitwaliwa kutoka kwao wakati huo.