Viongozi wakuu wa serikali wanakongamana katika mtaa wa South C, Nairobi kutathmini utendakazi wa serikali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mkutano huo unaongozwa na Rais William Ruto na unawaleta pamoja Mawaziri, Makatibu na maafisa wengine wakuu serikalini.
Akipigia debe mkutano huo, Rais Ruto ametaja tathmini na ari ya mashauriano kuwa muhimu katika kufanikisha ajenda ya serikali ya Kenya Kwanza ya kutekeleza mabadiliko ya kiuchumi kuanzia chini hadi juu, almaarufu BETA.
“Uangaziaji wa mara kwa mara wa utendakazi wa serikali utatusaidia kusughulikia mapungufu yetu na kuharakisha mafanikio yetu,” amesema Rais Ruto wakati akisisitiza umuhimu wa mkutano huo ambao pia unahudhuriwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Ni mkutano unaoandaliwa wakati Wakenya wanalalamikia gharama ya juu ya maisha ambayo kwa kiwango kikubwa imechangiwa na kupanda kwa bei ya mafuta.
Kiasi kwamba namna ya kushughulikia suala la gharama ya maisha imekuwa chanzo cha migawanyiko kati ya wanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Mamazungumzo inayoongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa Kimani Ichung’wah.