Home Habari Kuu Mkutano kuhusu tabia nchi na usalama waanza Nairobi

Mkutano kuhusu tabia nchi na usalama waanza Nairobi

0

Wadau katika maswala ya usalama na tabia nchi kutoka kote barani Afrika wanakongamana jijini Nairobi kwa ajili ya mkutano wa mwaka huu wa Berlin kuhusu Tabia Nchi na Usalama, yaani “Berlin Climate and Security Conference (BCSC).

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya kwa ushirikiano na wizara sawia ya Ujerumani na shirika la Adelphi. Adelphi ni shirika la Ulaya linalotoa ushauri kuhusu tabia nchi, mazingira na maendeleo.

Tangu kuasisiwa mwaka 2019, mkutano huo umeunganisha ulimwengu kupitia serikali mbalimbali, mashirika ya kimataifa, wataalamu na wasomi wa maswala ya mazingira na usalama.

Wote hao hushirikiana kushughulikia ipasavyo athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa amani na ulinzi na huwa wanatumia diplomasia, maendeleo na ulinzi.

Mkutano wa Nairobi utaangazia mifano bora kutoka Afrika, maendeleo ya ushirikishi wa wote kuhusu usalama wa tabia nchi na ushirikiano kati ya mipango kama vile ushughulikiaji wa tabia nchi kwa ajili ya amani endelevu na tabia nchi kwa ajili ya amani ili kuhakikisha kwamba maswala ya tabia nchi, amani na usalama yanapitiwa kipaumbele kabla ya kufanyika kwa mkutano mkubwa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka huu almaarufu COP28.

Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje Dkt. Korir Singoei anasema mabadiliko ya tabia nchi yanasalia kuwa changamoto kubwa enzi hii kwa sababu ni kikwazo kwa mazingira tunayotegemea na ni tishio kwa maisha ya binadamu na ya viumbe wengine.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here