John Kerry, mjumbe wa Amerika kuhusu tabia nchi yuko nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku nne ambayo ilianza Jumapili Julai, 16, 2023. Dhamira kuu ya ziara hiyo ni kufufua mazungumzo kuhusu kukabili ongezeko la joto ulimwenguni.
Haya yanajiri wakati ambapo joto limeongezeka maradufu katika eneo zima la kaskazini la ulimwengu.
Hii ndiyo ziara ya tatu ya ngazi za juu ya America nchini China mwaka huu wakati ambapo nchi hizo mbili zinajaribu kufufua uhusiano wao ulioharibiwa ushindani wa kibiashara, mvutano wa kijeshi na kulaumiana kuhusu ujasusi.
Waziri wa mambo ya nje nchini Amerika Antony Blinken na waziri wa fedha nchini humo Janet Yellen pia wamezuru China mwaka huu kujaribu kufufua uhusiano kati ya Amerika na China.
Mazungumzo ya pande mbili ya Kerry na mwenzake wa China Xie Zhenhua yataangazia maswala kadhaa kama vile kupunguza utoaji wa gesi ya methane, kupunguza matumizi ya makaa ya mawe, kuzuia ukataji wa miti na kusaidia nchi masikini kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kerry na Xie, ambao wana uhusiano mwema baada ya kuhudumu kama wajumbe wa nchi zao kwa muda huenda wakazungumzia hatua ya China ya kupinga ushuru wa Amerika na vikwazo vingine kuhusu uuzaji wa China nchini humo wa vifaa vya kuunda kawi kutokana na miale ya jua.
Nchi zote mbili zinatambua kwamba zinafaa kuweza kushirikiana katika maswala ya mabadiliko ya tabia nchi bila kuzingatia masuala mengine ambayo wamekosa kuelewana.