Misri itachuana na wenyeji Morocco katika fainali ya kuwania taji ya kombe la taifa bingwa barani Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 23 Jumamosi hii uwanjani Prince Moulay Abdellah jijini Rabat nchini Morocco.
Timu hizo mbili ziliandikisha ushindi kwenye michuano yao ya nusu fainali zilizoandaliwa jana usiku.
Mabingwa watetezi Misri waliilemea Guinea bao 1-0, bao lililofungwa na Mohamed Shehata ilhali Morocco iliishinda Mali mabao 4-3 kupitia kwa mikwaju ya penalti baada ya timu hizo mbili kutoka sare mabao 2-2 katika muda wa kawaida na ziada.
Zakaria El Ouahdi aliipa Morocco uongozi mnamo dakika ya 14 lakini Mali ikasawazisha katika dakika ya 66 kupitia kwa Mamady Diambou.
Morocco ilifunga bao la pili katika daika ya 108 kupitia kwa Amine El Ouazzani huku Mali ikisawazisha kupitia kwa Issoufi Maiga dakika nane baadaye na mchuano huo kumalizika sare ya mabao 2-2.
Mikwaju ya penalti ililazimika kupigwa ili kuamua mshindi ambapo wenyeji Morocco waliibuka na ushindi wa mabao 4-3.